Saturday, March 25, 2017

Wanawake wapigwa marufuku kushinikizwa kuandamana.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Loliondo wakiandamana kupinga kamati wa utatuzi wa mgogoro wa pori tengefu.


BAADHI ya Wanawake  pamoja na watoto  wanatumiwa kama chambo  kwaajili ya  kusimamisha msafara wa Kamati ya Kukamilisha mchakato wa Utatuzi wa  Mgogoro wa Matumizi ya Ardhi kwenye Pori Tengefu la Loliondo.

Kutumika kwa wanawake hao ambao baadhi yao walikuwa na watoto wadogo migongoni kumebainika jana wakati kamati hiyo ilipokuwa ikiendelea kuangalia maeneo mbalimbali ya Pori hilo Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita 15,000 za mraba zilizoleta mgogoro kwa zaidi ya miaka 25 sasa.

Wanawake hao katika Kata ya Malambo na Kata ya  Arash,ambao kwa pamoja walibeba mabango  ya kuisihi Kamati hiyo kutenda haki mengine
yakimtuhumu Waziri wa Maliaisili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
wakidai kuwapenda wanyamapori kuliko binadamu.


Baadhi ya wanwake hao ambao ni  Rehema Pascal na Lemnyaki John
walisimamisha mafara huo kwakuonyesha mabango yao yanayodai kutokubali kuhamishwa katika Pori hilo huku wengine wakipandisha mori na kupiga mayowe.


Baada ya Rc,Gambo kuyasoma mabango hayo aliwapa vipaza sauti ili
wayasome tena hapo ndipo waliposhindwa kuyasoma na kudai kuwa hawajui Kiswahili.
“Nani aliyewaandikia mabango haya wakati hamjui kusoma ,mnatumiwa na
viongozi wenu hukusu mgogoro huu ,msikubali kutumika maana hamjui
serikali inafanya hivi kwa nia ipi na wala serikali haina mpango wa
kuchukua ardhi hii bali tunachokifanya ni kujua hayo mnayoyasema yapo
kiuhalisia au la ili tukamilishe kazi yetu”.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Felex Wandwe alisisitiza
aliwatoa hofu wananchi wa Kata saba za wilaya hiyo kutokubali kutumika
vibaya kwaajili ya Pori hilo kwani serikali inachofanya hivi sasa ni
kuchukua mapendekezo ya kamati hiyo kisha kuyawasilisha kwa Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa .


“Msikubali kutumiwa kwa maslahi ya wengine sisi tupo pamoja na
wawakilishi wenu na kabla ya kuanza zoezi hili walijua tunakuja
kufanya nini hivyo mtulie”.
Pia Katibu wa Kamati hiyo, Bahati Chisanza alisema kuwa ni vyema
wananchi wakajua kuwa serikali haichukui ardhi bali inachokifanya ni
kutaka kupanga matumzii bora ya ardhi ili kila mtu anufaike nayo.


Awali Mwenyekiti wa Kijiji cha  Malambo, Lazaro Mashele alitoa rai kwa
kamati hiyo kutoiingiza Kata hiyo ya Malambo katika matumizi bora ya
ardhi kwani kata hiyo haina mgogoro na Pori hilo bali ni wahifadhi
wazuri wa wanyamapori ingawa kata hiyo ni sehemu ya mazalia ya
wanyama.


“Tunawaomba wakuu kata hii isiingizwe katika  mgogoro huu kwani hatupo
ndani ya vijiji saba lakini pia kata hii inatumika kwaajili ya mazalia
ya wanyamapori ambao hatuna ugomvi nao”.


Aidha  Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo alisisitiza kuwa wamechukua maoni ya mwenyekiti huyo na watafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na
wananchi hao ,wahifadhi na wataalam wa ardhi kisha kuyawasilisha kwa
Waziri Mkuu Machi 25 mwaka huu.


Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo
alitoa rai kwa wananchi hao  kutokubali kutumika kwa msalahi ya
wengine na kutoa rai kwa viongozi wa vijiji,madiwani na mashirika
yasiyo ya kiserikali kuacha mara moja kuwatumia wananchi kwaajili ya
kuwapotosha kuhusu Pori Tengefu la Loliondo.


Pia alisema polisi wataanza msako kwa wale wote ambao si raia wa
Tanzania wanaoishi Wilayani Loliondo huku akisisitiza kuwa wamemkamata
mtu mmoja ambaye ni mwanaume (hakumtaja jina) kwa kufanya vurugu
wakati kamati hiyo ilipokuwa ikifanya kazi yake katika kata mbalimbali
na muda wowote atafikishwa mahakamani wilayani humo.



0 comments:

Post a Comment