Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, imeiagiza bodi ya
Mamlaka ya maji safi na Usafishaji Mazingira ya jiji la Arusha AUWSA kuweka
kipaombele katika utunzaji wa vyanzo vya maji viliyopo katika mlima Meru.
Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maji
katika jiji la Arusha.
“Nimewahi kusikia wataalam wa maji wakisema Vita ya Tatu
ya dunia itahusisha kugombea maji,ninaomba sisi tuanze kujihami kwa kutunza
vyanzo vyetu vya maji.Niitake bodi ya AUWSA kuandika andiko la mradi ambalo
tutalipigia debe katika ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Mazingira ili
kuweza kupata ufadhili wa kampeni yetu hii ya utunzaji wa vyanzo vya maji”.
Gambo alisema,itakuwa haina maana kutumia kiasi kikubwa
cha fedha za serikali katika uboreshaji wa huduma za maji na baada ya miaka michache
ijayo vyanzo vyote vikauke.
Nae Mkurugenzi wa Mmlaka ya Maji safi na usafirishaji (AUWSA)
Mhandisi Ruth Koya amesema, mradi huo utakamilika June 2020 na Arusha
itanufaika sana na mradi huo kwakuwa
ukosefu wa maji utakuwa historia.
Amesema tayari wakandarasi wameshaanza kusambaza mtandao
wa maji safi na taka kwa kuweka mabomba ya kisasa yanayoendana na mahitaji ya
sasa.
Aidha, amesema mpaka mradi huu ukamilike upatikanaji wa
maji katika jiji la Arusha utafikia asilimia 100 tofauti na hali ya sasa ambapo
ni asilimia 44 tu ya wananchi ndio wanapata maji safi.
Ruth alisema, uzalishaji wa maji utaongezeka kutoka
wastani wa lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku na upotevu wa maji
utashuka toka asilimia 40 za sasa hadi wastani wa asilimia 25.
Mwenyekiti wa bodi ya AUWSA, Dk. Richard Masika
ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kutoa fedha kiasi cha shilingi
bilioni 520 kupitia mkopo wa riba nafuu kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) katika kufanikisha mradi huu mkubwa na ametoa rai kwa wananchi wa Arusha
kuitunza muindombinu iliyopita katika maeneo yao kwa ajili ya manufaa ya leo na
baadae.
Gambo yupo katika ziara ya siku 3 katika wilaya ya
Arusha, Arumeru na Longido akikagua miradi ya maji inayoendeleo katika maeneo
hayo.