Friday, November 23, 2018

TUNZENI VYANZO VYA MAJI

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, imeiagiza bodi ya Mamlaka ya maji safi na Usafishaji Mazingira ya jiji la Arusha AUWSA kuweka kipaombele katika utunzaji wa vyanzo vya maji viliyopo katika mlima Meru.

Ameyasema hayo alipokuwa  katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maji katika jiji la Arusha.

“Nimewahi kusikia wataalam wa maji wakisema Vita ya Tatu ya dunia itahusisha kugombea maji,ninaomba sisi tuanze kujihami kwa kutunza vyanzo vyetu vya maji.Niitake bodi ya AUWSA kuandika andiko la mradi ambalo tutalipigia debe katika ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Mazingira ili kuweza kupata ufadhili wa kampeni yetu hii ya utunzaji wa vyanzo vya maji”.

Gambo alisema,itakuwa haina maana kutumia kiasi kikubwa cha fedha za serikali katika uboreshaji wa huduma za maji na baada ya miaka michache ijayo vyanzo vyote vikauke.
 Nae Mkurugenzi wa Mmlaka ya Maji safi na usafirishaji (AUWSA) Mhandisi Ruth Koya amesema, mradi huo utakamilika June 2020 na Arusha itanufaika sana na mradi huo kwakuwa  ukosefu wa maji utakuwa historia.

Amesema tayari wakandarasi wameshaanza kusambaza mtandao wa maji safi na taka kwa kuweka mabomba ya kisasa yanayoendana na mahitaji ya sasa.

Aidha, amesema mpaka mradi huu ukamilike upatikanaji wa maji katika jiji la Arusha utafikia asilimia 100 tofauti na hali ya sasa ambapo ni asilimia 44 tu ya wananchi ndio wanapata maji safi.
 Ruth alisema, uzalishaji wa maji utaongezeka kutoka wastani wa lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku na upotevu wa maji utashuka toka asilimia 40 za sasa hadi wastani wa asilimia  25.

Mwenyekiti wa bodi ya AUWSA, Dk. Richard Masika ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 520 kupitia mkopo wa riba nafuu kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kufanikisha mradi huu mkubwa na ametoa rai kwa wananchi wa Arusha kuitunza muindombinu iliyopita katika maeneo yao kwa ajili ya manufaa ya leo na baadae.

Gambo yupo katika ziara ya siku 3 katika wilaya ya Arusha, Arumeru na Longido akikagua miradi ya maji inayoendeleo katika maeneo hayo.


0 comments:

Post a Comment