Wednesday, August 29, 2018

MWANAUME JALI AFYA YAKO, PIMA

Mkuu wa Wilaya  ya Monduli Idd Kimanta (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali na wadau wa sekta ya afya katika uzinduzi wa kampeni ya "Furaha Yangu",Meserani wilayani Monduli.

Watakaogundulika wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI wanatakiwa kuwaleta wenza wao wapimwe  pia ili waweze kujitambua na kuishi mda mrefu.

Ameyasema hayo Mkuu wa Wilaya ya Monduli  Idd Kimanta kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo katika uzinduzi wa kampeni ya upimaji wa virusi vya UKIMWI kwa hiari ijulikanayo kama “FURA YANGU”.

Gambo amesema bado idadi ya wanaume wanaoenda kupima ni ndogo sana ukilinganisha na wanawake, hivyo nguvu za uhamasishaji inaitajika zaidi kwa wanaume.

Ikiwezekana hata kutumia mikusanyika kama sehemu za ibada na maeneo ya starehe ili kuweza kuwapata wanaume wengi na kuwahamasisha wajitokeze zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Idd Kimanta akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu akiwa na (kulia) ni Mganga Mkuu wa Wilaya Dr. Titus Mmasi, wilayani Monduli.

Pia wataalamu wanatakiwa kuongeza zaidi wigo wa utoaji huduma hii kama kutoa ushauri nasaha na kuwahamasisha wagonjwa wapime kwa hiari.

Akitoa takwimu za hali ya maambukizi kwa mkoa wa Arusha Mganga mkuu wa mkoa Vivian Wonanji, amesema kwa mwaka 2011/2012 hali ya maambukizi imeshuka sana kutoka 3.2% hadi 1.9 kwa mwaka 2017/2018.

Amesema hali hii ni nzuri sana kwa mkoa wetu lakini hatutakiwi kupunguza nguvu hii ya upimaji wa hiari na matumizi ya dawa kwa wagonjwa kwani mpaka sasa waliogundulika na VVU ni 52.2% wenye umri kati ya miaka 15-64 ambapo wanaume ni 45.3%na wanawake ni 55.9%.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Idd Kimanta akipata maelezo kutoka kwa mganga mkuu wa Wilaya ya Monduli Dr. Titus Mmasi wakati wa kutembelea mambanda mbalimbali ya upimaji wa kampeni ya Furaha Yangu,Wilayani Monduli.

Hali hii inaonesha kuwa bado jitihada inaitajika kuhamasisha wanaume wajitokeze zaidi katika upimaji na sio upimaji tu hata pia matumizi ya dawa kwani kati ya wagonjwa 90.9% wanaotumia dawa wanaume ni 86.2% tu na wanawake ni 92.9%.

Aidha, amesisitiza zaidi hata katika hatua ya kufubaisha VVU kwa wagonjwa wanaotumia dawa bado msukumo ni mdogo kwa wanaume kwa 84% kati ya wagonjwa 87.7%.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Idd Kimanta akipima msukumo wa damu (Presha) kama ishara ya uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu, Wilayani Monduli.

Kupitia kampeni hii ya Furaha yangu yenye ujumbe wa Pima,Jitambue,Ishi itasaidia zaidi kuwahamasisha wanaume kupima kwa hiari.

Akitoa takwimu za upimaji katika kampeni hii kuanzia Agosti 17, 2018 wilayani Monduli mwakilishi kutoka Mkapa Foundation David Mnkhally amesema,jumla ya watu 5,730 ndio wameweza kupima na 29 ndio wamegundulika na maambukizi ya VVU.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Idd Kimanta akizungumza na wananchi wa Meserani (Hawapo Pichani) katika uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu,Wilayani Monduli.

Ikiwa katika kata ya Monduli Juu jumla ya watu 2.987 wamepima na kati yao wanaume ni 1,206 sawa na 40.3% na wanawake ni 1,781 sawa na 59.6% na kata ya Meserani waliopima ni 2.743,wanaume ni 1,378 sawa na 50.2% na wanawake ni 1,365 sawa na 49.7%.

Kampeni hii ya Furaha Yangu ilizinduliwa rasmi mnamo Juni 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dodoma, na kwa mkoa wa Arusha zimezinduliwa rasmi Agosti 28, 2018 katika kata ya Meserani wilayani Monduli na itaendelea katika wilaya ya Ngorongoro.

Mganga Mkuu wa Mkoa Dr. Vivian Wonanji akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya "Furaha Yangu" Wilayani Monduli.


Mwakilishi kutoka Taasisi ya Mkapa Foundation David Mnkhally akisoma taarifa fupi kwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya "Furaha Yangu",Wilayani Monduli.


0 comments:

Post a Comment