Friday, September 16, 2016

MKUU WA MKOA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UTUME WA KANISA LA WAADVENTISTA WA SABATO


  Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(katikati) akiongozwa na vijana wa Skauti kwenda kukagua mabanda ya taasisi za kanisa la waadventista wa Sabato Tanzania

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo  akikagua mabanda yenye vitabu na majarida mbalimbali yanayochapishwa na taasisi za kanisa la wasabato Tanzania,kushoto ni Mchungaji Eliasi Ijiko.

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(katikati) akikata utepe kama ishara ya maadhimisho ya maiaka 50 ya Utume Burka,kushoto ni Mch. Mchungaji Eliasi Ijiko na kulia ni Askofu Godwin Godwin Lekundayo

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akisoma  hotuba yake kwa viongozi na waumini wa waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(katikati) na viongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika picha ya pamoja.
Viongozi wa dini nchini wameombwa kuhamasisha waumini wao kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi ili kuongeza kasi ya kuleta maendeleo katika Taifa la Tanzania na pia wametakiwa kuhamasisha waumini wao kuhakikisha wanadai risiti kila wanapoenda kununua bidhaa au  kupata huduma mbalimbali.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa  na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr John Joseph Pombe Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya miaka 50 ya Utume wa Kanisa la Waadventista wa Sabato.

Akizungumza na waumini na viongozi wa Kanisa hilo lililopo Burka mjini hapa, Mkuu wa Mkoa Arusha Gambo alisema, Watanzania wanalojukumu la kufanya kazi kwani hata  Vitabu vya Dini vimeelekeza kuwa mtu asiyefanya kazi na asile na mafundisho hayo ya dini yanaendana na falsafa ya hapa kazi tu.

Mhe. Gambo aliendelea kusisitiza kwamba kutokana na maelekezo hayo ya vitabu vya dini ni wazi kwamba kila mtu anatakiwa kufanya kazi kwa kadiri ya uwezo aliopewa na Muumba ili apate riziki hatua itakayowezesha pia kupunguza wategemezi katika Taifa letu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo RC Gambo kwa niaba ya Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni vyema kwa kila mmoja wetu kufanya kazi na kulipa Kodi.

"Kwa yule ambaye hatalipa Kodi ajue kwamba anaikosesha nchi yake mapato ambayo yangeweza kutumika kuendesha shughuli mbalimbali za maendeleo, pia tutambue kwamba huduma zote ni gharama na zinatokana na kodi tunazolipa. 
Hivyo katika Serikali ya Awamu ya Tano asiyefanya kazi na asile na zaidi ya hapo asiyelipa kodi ni vyema akafahamau kwamba analirudisha taifa lake nyuma. Niwaombeni sana viongozi wa Dini muhamasishe waumini walipe kodi kwa mustakabali wa Taifa letu"

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni Mch. Geofrey Mbwana akitoa somo fupi wakati wa maadhimisho hayo alisema amefurahishwa sana na uteuzi wa Mhe. Gambo na ana imani na vijana kwa sababu vijana wakati wao ni sasa na pia ni taifa la leo hivyo wakipewa nafasi kama hii hudhihirisha vipawa vilivyomo ndani yao na bila shaka Mkoa wa Arusha utakua Mkoa kielelezo kwa Taifa hili.

Kanisa hili la Sabato katika Tanzania lilianzishwa Katika kijiji cha Giti kilichopo Mamba Miamba huko Same mnamo mwaka 1903 na kuendelea kukua katika Mji wa Shirati Mara na kisha kufika Arusha na kuanzisha Kanisa la Burka mwaka 1966 likiwa na Jengo moja dogo na waumini nane tu.

Hivi sasa Kanisa hili lina majimbo mawili na waumini zaidi ya 500,000 Tanzania. Kanisa hili pia wanamiliko Chuo Kikuu kimoja, Shule za Sekondari 17, Msingi 11 na shule za awali 11. Pia Kanisa hili lina Hospital moja, Kituo cha Afya kimoja na Zahanati 28.

RC Gambo aliendelea kuwaomba viongozi mbalimbali wa dini wazidi kumuombea na kumtia Moyo Mhe. Rais katika kazi yake ngumu na kubwa anayoifanya kwa maslahi ya Taifa haswa kusaidia wanyonge ambao kwa muda mrefu hawakuwa sehemu ya Agenda kubwa ya Serikali. Pia waendelee kuwasisitiza wanasiasa watambue kuwa wakati wa Siasa  umekwisha ni vyema Mhe. Rais akapewa nafasi ya kuwatumikia watanzania kwa yale aliyoyaahidi kupitia utekelezaji wa ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI na watakutana tena kwenye siasa mwaka 2019 - 2020.

0 comments:

Post a Comment