Wednesday, September 7, 2016

WATAKAO HUJUMU MISAADA WATAWAJIBISHWA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo,amewataka watumishi wote wa Mkoa wa Arusha kutekeleza wajibu wao kama watumishi na kuachana na mambo ya siasa ambayo yanarudisha maendeleo yawananchi nyuma.
Ameyasema hayo alipokuwa akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro alipofanya ziara ya siku moja Wilayani humo na kukutana na changamoto mbalimbali zikiwepo za migogoro ya ardhi.

Muheshiwa Gambo ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha inatatua migogoro yote ya ardhi na ile inayoshindikana kwa ngazi hiyo ndio ipelekwe kwenye ngazi ya Mkoa na yeye atakuwa tayari kuwasaidia.

Aidha ametaka kupewa ripoti ya fedha zinazotolewa na wafadhili katika kila Halmashauri napia zile zinazopelekwa kwa wafugaji zielezwe matumizi yake na yeye atapita kukagua hizo shughuli za maendeleo kwa wananchi ili ajiridhishe na matumizi yake kama ni halali au sio.

Alisema anataka kupata pia taarifa juu ya chakula kinachotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa wananchi wa Wilaya hiyo kama kweli kinawafikia wahusika hususani wananchi wa hali ya chini.

"Ikibainika kuwa fedha za wafadhili na chakula cha msaada vyote vinatumika visivyo basi wahusika wajiandae kuwajibishwa ipasavyo, kwasababu tunatakiwa kuwatendea haki wananchi wetu na sivinginevyo",alisema Gambo.

Aidha aliwaomba wawekezaji wakishirikiana na madiwani waendelee kudumisha uhusiano mzuri baina ya wananchi na wawekezaji hao ili kwa pamoja maendeleo kwa wananchi yapatikane kwa wakati.

Muheshiwa Gambo alikuwa na ziara ya siku moja katika Wilaya ya Ngorongoro kwalengo lakufuatilia shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.

Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo(Hayupo Pichani) alipowatembelea katika ofisi za Wilaya.

0 comments:

Post a Comment